Ticker

6/recent/ticker-posts

Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani kutikisa JNICC leo

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mashindano ya Utanashati, Urembo na Mitindo ya Viziwi Duniani ambayo yanafanyika nchini.
Mashindano hayo ya 12 duniani yanafanyika leo Oktoba 29, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika na Tanzania kuwa wenyeji wa kwanza.

Hayo yamesemwa Oktoba 28, 2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbas wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Ni mbele ya Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo ikiongozwa na Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani (MMDI),Bi.Bonita Ann Leek ambapo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa naye atakuwa mgeni maalumu.

"Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa aungane nasi, lakini kutokana na majukumu mbalimbali, Mheshimiwa Rais atawakilishwa na Mheshimiwa Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

"Mashindano haya sio jambo dogo ni jambo kubwa sana, watu wengi wako hapa na mpaka sasa Mheshimiwa Rais wetu amekubali jambo hili kubwa kufanyika hapa nchini kwetu,"amebainisha Dkt.Abbas.
Dkt.Abbas amebainisha kuwa, Serikali pia imewapa zawadi washindi wote wa shindano hilo la kidunia na viongozi wao kutembelea mbuga ya wanyama ya Ngorongoro Oktoba 31,2022 baada ya kumalizika kwa mashindano hayo kesho ikiwa ni mwendelezo wa Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Abbas amefafanua kuwa, miongoni mwa sababu zinazoendelea kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuaminika na kupewa kipaumbele katika masuala mbalimbali duniani achilia mbali ukarimu, umoja na upendo ni pamoja na utulivu na amani ambayo imetawala kila mahali.

Pia amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali kuanzia Bara na Visiwani ambavyo kila mgeni akivisikia anatamani kufika ili kuja kufurahia maisha.

"Hapa Tanzania tumejaliwa kuwa na vivutio vingi kuna Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine mbalinbali ya vivutio vizuri vya kwenda kurelax. Kwa Tanzania tangu mashindano haya yaanze kufanyika, Tanzania ni nchi ya 12 na kwa mara ya kwanza mashindano haya yalifanyika Las Vegas nchini Marekani mwaka 2010,"amesema.

Amesema, tukio hilo ambalo linatarajiwa kufuatiliwa na mamilioni ya watu ndani na nje ya nchi litawakusanya pamoja wageni zaidi ya 1,400 ukumbuni hapo na litarushwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari huku likisindikizwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.

"Na niwaambie tu, katika tukio hilo itaanza kuoneshwa filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ili watu waweze kuona jinsi Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii,"ameeleza Dkt.Abbas.

Serikali inajali

Wakati huo huo, Dkt.Abbas amesema,Serikali itaendelea kukuza vipaji na vipawa mbalimbali walivyonavyo watanzania, pili kuheshimu na kulinda na kuendeleza vipaji na vipawa vya Watanzania wenye changamoto mbalimbali za ulemavu.

"Pia tuna sheria za nchi zinawalinda, kutunza haki zao na tuna sera, majengo yanayowawezesha kupata huduma na mikakati mbalimbali imewekwa na Serikali yetu ili kuwapa nafasi kwenye nyadhifa mbalimbali za uongozi.

"Kwa hiyo Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kuwaunga ndugu zetu hawa mkono. Mnafahamu kuna timu yetu ilienda mpaka Uturuki ikashiriki michezo ikafika mpaka robo fainali na wameitangaza Tanzania vyema duniani. Kwa wale wanaoshiriki michezo Serikali inawasapoti sana, viziwi pia Serikali inawasapoti sana kwa kila hatua njema.

"Kule Uturuki, tulianza kucheza na Hispania tukatoana nao bila kwa bila, tukacheza na Poland kwa tabu sana wakatufunga 3-0, akaja Mjapan tukamtandika bao 2, wakaja Waitaliano tukawapiga, Mwenyezi Mungu wa ajabu sana na ni mwingi wa rehema. Kuna wenzetu wazima, lakini hawawezi kufanya mambo makubwa kama haya. Kwa hiyo Serikali itaendelea kuwaunga mkono,"amefafanua.

Lugha ya alama

Katibu Mkuu Dkt.Abbas amesema, "Lugha ya alama ni jambo ambalo Serikali kwenye programu zake mbalimbali imekuwa ikilifanya ili kuwasaidia wenzetu waendelee kuwasiliana na katika vyuo vikuu kuna programu kabisa wenzetu wanasoma.
"Wataalam kila mwaka wanakuja kusaidia, wameweka departments (idara) au units (vitengo) kabisa za special needs (wenye mahitaji maalumu), special education (elimu maalumu) kadri tunavyozidi kuwabaini na Mheshimiwa Rais kesho kutwa atatangaza matokeo ya Sensa...itakuja kusaidia kujua viziwi wangapi ili kuongeza idadi ya wataalam," amesema.

"Hata sisi kwenye haya mashindano tulitaka wakalimani...kwenye lugha ya alama wapo wakalimani wa Kimataifa na wakalimani wa Tanzania, jinsia wewe unavyomwelezea Rais Samia ni tofauti na wanavyofanya Kimataifa.

"Pia Tanzania tunacreate symbols (alama) zetu na wenzetu kumbe wana symbols (alama) zao kwa hiyo hawa wakalimani wetu pia wamefundishwa jinsi ya kufahamu symbols.

"Hata sisi kwenye haya mashindano wenzetu Watanzania tumewasaidia kujua, kwa hiyo serikali inaendelea kuwasaidia na kuweka mazingira mazuri kwa wenzetu viziwi wote na wengine wenye changamoto tutaenzi vipaji vyao ili waendelee kuonesha vipaji vyao na maandalizi yote hapa yametimia.

"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania niwashukuru MMDI (Miss & Mister Deaf International, Inc) kwa kuiamini Tanzania na kuleta mashindano haya hapa Tanzania," amesema Dkt.Abbas.

Rais Leek

Kwa upande wake Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani (MMDI),Bi.Bonita Ann Leek amesema, miongoni mwa sababu zilizowashawishi kuyaleta mashindano hayo hapa Tanzania ni pamoja na ukarimu, upendo na umoja wa Watanzania.
Pia amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejitengenezea heshima ya kipekee katika uso wa Dunia kutokana na namna ambavyo inajali utu, amani na utulivu. "Hivyo ni vigezo muhimu sana na kwa kweli hayo yote tumeyashuhudia hapa, asanteni sana Watanzania,"amesema Rais Leek.

Mrope

Naye Rais wa Mashindano ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Afrika (MMDAF),Habibu Mrope amesema kuwa,maandalizi ya mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika kesho jijini Dar es Salaam yamekamilika.

"Tuna mahusiano mazuri sana na Serikali yetu chini ya uongozi wa Rais Samia na Serikali imetujengea mahusiano mazuri kupitia Rais Samia Hassan.

"Serikali ndio chombo chenye nguvu kimeendelea kutusapoti sisi walemavu mpaka hapa tumefikia ametupa heshima kubwa pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kila kitu tukiomba anakubali, kila jambo linakwenda, tunasema asante sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutupa nafasi hii na kukubali jambo hili lifanyike hapa nchini. Pia tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mchengerwa kwa ushirikiano wake amebeba dhamana kuongoza hii wizara.

"Tunawakaribisha hapa Tanzania nchi yenye amani hapa ni nyumbani, tunawashukuru sana vile vile ninamshukuru Mheshimiwa Abbas, Katibu Mkuu kwa ushirikiano huu mzuri na pia Mheshimiwa Mkurugenzi Ishengoma (Dkt.Emanuel Ishengoma) tumekuwa tukiwasiliana hata usiku, nawashukuru maofisa wa Wizara ya Utamaduni na Michezo na vyombo vyote vya habari kwa ushirikiano wenu,"amesema Mrope.

Post a Comment

0 Comments