Ticker

6/recent/ticker-posts

Uchaguzi Mwenyekiti UWT Simanjiro Kurudiwa


Na Mwandishi wetu, Simanjiro


UCHAGUZI wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa wanawake wa CCM Tanzania UWT Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara unatarajiwa kurudiwa upya Oktoba 15.


Katibu wa UWT wilaya ya Simanjiro, Leokadia Fisoo amesema uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa tena jumamosi ijayo ya Oktoba 15.


Fissoo amesema uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa mara baada ya mmoja kati ya wagombea wa nafasi hiyo kukata rufaa ngazi ya UWT Taifa.


Amesema malalamiko ya mgombea huyo yameonekana ni sahihi hivyo uchaguzi huo utarudiwa upya kwenye nafasi moja ya Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Simanjiro.


"Uchaguzi utarudiwa jumamosi ijayo na nimeshawapa taarifa wajumbe wa kata husika na wajumbe wa wilaya juu ya kurudiwa kwa uchaguzi huo," amesema Fissoo.


Amewataja watakaogombea nafasi hiyo ni wale waliopitishwa na halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Manyara ambao ni Agnes Brown, Anna Shinini, Naomi Edward na Rehema Yohana.


Awali, uchaguzi wa UWT wilaya ya Simanjiro ulifanyika Septemba 24 mwaka huu ambapo kwa nafasi hiyo ya Mwenyekiti ililazimika kurudiwa mara mbili.


Katika uchaguzi huo matokeo yalikuwa Anna Shinini aliongoza kwa kupata kura 97, Agnes Brown 86, Naomi Edward 10 na Rehema Yohana 2.


Hata hivyo ikabidi uchaguzi huo urudiwe tena kutoka a na mshindi kutokupata zaidi ya asilimia 50 na matokeo yakawa Agnes kura 99 na Anna kura 96.


Post a Comment

0 Comments