Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS KUADHIMISHA SIKU YA VIPIMO MEI 30,2023 JIJINI ARUSHA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewakaribisha wadau mbalimbali kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vipimo ambayo TBS inatarajia kusherekea Mei 30,2023 mkoani Arusha yenye kauli mbiu "VIPIMO VINAVYOUNGA MKONO MFUMO WA CHAKULA DUNIANI".

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24,2023 Jijini Dar es Salaam, Afisa Metrolojia TBS, Bi.Angela Charles amesema kwa mwaka huu katika kusheherekea Siku ya Vipimo Duniani, wanaangalia dhana nzima ya upatikanaji wa chakula kutokana na ongezeko la watu Duniani.

Amesema mabadiliko ya hali ya hewa yameleta changamoto katika upatikanaji wa chakula hivyo basi kupitia kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ya vipimo duniani, wanaangalia upatikanaji wa chakula pamoja na umuhimu wa vipimo katika mnyororo mzima wa thamani kwenye chakula kuanzia shambani hadi kumfikia mlaji.

Aidha amesema katika maadhimisho hayo wanategemea kuwa na Mada mbalimbali pamoja na kuwatembelea wadau wao walipo mkoani Arusha kwaajili ya kuendelea kutoa elimu ya namna ya kufanya vipimo sahihi na namna ya kupata na kutumia huduma zinazotolewa na TBS.

Kwa upande wake Mmetrolojia Mkuu, Kitengo cha Maabara ya Metrolojia TBS, Bw.Joseph Mahilla amewataka wananchi kuzingatia vipimo ambavyo ni sahihi katika hatua za uzalishaji wa chakula kuanzia shambani hadi kumfikia mlaji.

Hata hivyo amewataka wananchi kuhakikisha mbegu ambazo wanazitumia katika uzalishaji ni zile ambazo zimethibitishwa ubora.

"Kutokana na kauli mbiu ya mwaka huu, tuaanza kuangalia vipimo kuanzia mwanzo wa mfumo wote wa chakula, utaanzia kwenye maabara ya utafiti ambao unaangalia ni aina gani wa udongo unafaa kwaajili ya zao fulani". Amesema Bw.Mahilla.


Mmetrolojia Mkuu, Kitengo cha Maabara ya Metrolojia TBS, Bw.Joseph Mahilla akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24,2023 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam
Afisa Metrolojia TBS, Bi.Angela Charles akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 24,2023 katika Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam


Post a Comment

0 Comments