Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WA UTALII WAMPA TANO MHE.RAIS, WASIFU KASI YA WIZARA



Na John Mapepele


Wadau wa Sekta ya Utalii nchini wametumia mkutano wao na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mabadiliko chanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake, huku wakisifu kasi ya sasa ya utendaji wa Wizara.

Wadau hao wa utalii takribani mia sita kutoka katika vyama vyote vya wadau wa utalii nchini wameyasema hao usiku wa kuamkia leo mei 27, 2023 katika mkutano maalum na Wizara ya Maliasili na Utalii uliochukua zaidi ya masaa nane na kumalizika saa sita usiku, ulioratibiwa na Wizara ya Maliasili ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiambatana na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi na Naibu wake Anderson Mutatembwa ameongoza menejimenti ya Wizara na taasisi zote zilizochini ya wizara hiyo kufanya kikao maalum na wadau hao.

Kikao hicho ambacho Mhe. Mchengerwa ndiye Mwenyekiti kimekuwa na lengo mahususi moja tu la kujadili changamoto mbalimbali za kisekta na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu ili kuboresha sekta huku watendaji wakitakiwa kujibu hoja zote za wadau.




Akichangia hoja katika mkutano huo, Mwenyekiti wa waongoza utalii kanda ya kaskazini (NTSGS) Qorro Englebert amempongeza Rais Samia kwa kutumia kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa uviko 19 kuwapatia mafunzo maalum wadau wa utalii zaidi ya 1000 katika vyuo vya Serikali ambayo amedai yamesaidia kuwaongezea ujuzi maalum katika kazi zao za kila siku.

Ameiomba Serikali kuwapa upendeleo maalum wanafunzi wanaomaliza mafunzo maalum ya uaskari wa uhifadhi katika vyuo vya Serikali ili waweze kutumia taaluma hiyo waliyoisomea badala ya kuajiri askari wasiyokuwa na elimu ya uhifadhi.

Pia amempongeza Mhe. Rais kwa kupunguza kodi za kutua ndege na kufafanua kuwa baada ya punguzo hilo kumekuwa na matokeo chanya ya wimbi kubwa la ndege kuwaleta watalii.

Aidha wadau hao wamepongeza uongozi mpya kwa kuonesha kasi mpya ya ufanyaji kazi huku wakisifu namna Waziri Mchengerwa anavyoshirikiana na watendaji wake katika shughuli mbalimbali huku wakifafanua kuwa ushirikishwaji baina ya watendaji wa Wizara na wadau ni nguzo muhimu katika kuleta mafanikio ya haraka kwenye sekta.

“Naomba niwe mkweli Timu ya sasa hivi haijawahi kutokea. Katika kipindi kifupi tangu kuteuliwa kwenu tumeshuhudia Mhe. Waziri na Katibu Mkuu mmekuwa pamoja katika utendaji wenu wa kazi jambo ambalo limetupatia moyo, kwa kasi na ushirikishwaji huu na jinsi ambayo mmeanza vizuri tunatarajia mtatufikisha mbali.” Amesisitiza Mwenyeki Wile Chambulo ambaye ni Mwenyekiti wa TATO nchini.

Awali akifungua mkutano huo, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa katika kipindi hiki Serikali itakuwa karibu na wadau kwenye kila hatua ili kuhakikisha sekta inasonga mbele kwa maslahi ya wadau na taifa kwa ujumla.

“Kwa kushikiana na wadau na Serikali mtegemee maboresho makubwa yanakuja, na kamati yetu nataka ifanye kazi na ije na mapendekezo ili marekebisho haya yaweze kufanyika haraka.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Pia amesema katika kipindi hiki Serikali itaboresha miundo mbinu ikiwa ni pamoja na kuweka barabara za kiwango cha lami itakayokuwa inapitika mwaka mzima pamoja, pia kuimarisha ulinzi kwa mgeni.


Akifafanua mchango wa sekta ya utalii amesema Sekta hii ni miongoni mwa sekta muhimu na yenye mchango mkubwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi wetu, kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine muhimu.

“Mathalan, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2022 mchango wa sekta hii ulikuwa takribani asilimia 17 ya pato la Taifa, ambapo idadi ya watalii iliendelea kuongezeka kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1,454,920 kwa mwaka 2022. Mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 2.5 mwaka 2022. Kadhalika, sekta hii ilitoa fursa za ajira takribani milioni 1.5 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja." Ameongeza Mhe Mchengerwa

Amesema mafanikio hayo yanatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa kipaumbele sekta hii kupitia uwekezaji wa aina mbalimbali alioufanya pamoja na ushirikiano imara uliopo baina ya sekta za umma na Sekta Binafsi.

Post a Comment

0 Comments