Ticker

6/recent/ticker-posts

TBS Yashika Nafasi ya Pili Mchezo wa Kuvuta Kamba SHIMMUTA

SHIRIKA la Viwango Tanzania(TBS) limefanikiwa kupata kombe la mshindi wa pili kwa mchezo wa kuvuta kamba katika mashindano ya SHIMMUTA ambayo yamefanyika Jijini Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa habari Nov 25,2023, Mwenyekiti wa michezo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. Lucas Gwila amesema kuwa moja ya sababu ya mafanikio yao kufika hatua ya fainali katika mashindano hayo ni suala la nidhamu kwa timu nzima pamoja na ushirikiano.

"Siri ya mafanikio yetu ni suala la nidhamu, ushirikiano na ushiriki wa mara kwa mara kwenye mabonanza yanayofanyika kwenye taasisi, kufanya mazoezi na kuchagua wachezaji wazuri". Amesema

Aidha Bw. Gwila amesema kuwa moja ya sababu iliyotia chachu mafanikio yao ni pamoja na kuwa na mbinu za ushindani, na kushindwa kwao kutwaa ubingwa kumesababishwa na kuzidiwa mbinu, ameahidi kwa mashindano yajayo watajitahidi kuchukua ubingwa kutokana na uzoefu walioupata.

"Mwakani timu yetu ya mashindano ya kamba ya TBS, naahidi tunaenda kuchukua ubingwa,nadhani wametuzidi kwenye mbinu ndogo ndogo". Ameeleza Bw. Gwila.

Amesema mashindano ya SHIMMUTA yanazidi kuwa bora zaidi kila mwaka ambapo kwa mwaka 2023 imekadiriwa zaidi ya watu 4000 wamejitokeza kuhudhuria na kushiriki katika mashindano hayo.

SHIMMUTA ni miongoni mwa Mashirikisho manne ya michezo yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere mnamo mwaka 1967 ambapo yanahusisha Mashirika ya Umma, Taasisi na makampuni binafsi Tanzania katika michezo kwa kusudi la kujenga mahusiano mema kitaasisi.

Post a Comment

0 Comments