Ticker

6/recent/ticker-posts

JUKWAA LA MAPROFESA LAJIPANGA KUINUA TAALUMA OUT

Jukwaa la Maprofesa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), limejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa linachangia katika kuinua na kuimarisha shughuli zote za kitaaluma, tafiti na huduma za ushauri wa kitaalamu zinazosimamiwa na chuo hiki kwa manufaa mapana ya taifa letu.

Azma hii imefikiwa kwa pamoja na wajumbe wa jukwaa hilo wakati wa mkutano wake wa tatu ambapo wajumbe wa jukwaa hilo wamekutana kuanzia Februari 15 hadi Februari 17 katika kampasi ya chuo cha Uongozi cha Mwl. Julius Kambarage Nyerere kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Akiongea wakati wa kufunga jukwaa hilo, kiongozi wa jukwaa ambaye pia ni naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Huduma za ushauri wa kitaalamu Prof. Deus Ngaruko, amesisitiza kuwa jukwaa hili ndiyo sehemu pekee wanazuoni wanaweza kukaa na kujadili mambo yao kwa utulivu na kufikia mikakati ambayo italeta tija kwa taasisi na taifa letu.

“Tumejadiliana na kukubaliana mengi lakini kinachotakiwa sasa ni kushirikiana na taasisi, makampuni na wanataaluma wenzetu wote ndani ya chuo na popote ulimwenguni katika kuandika na kusimamia miradi itakayosaidia kuinua na kuboresha maisha ya jamii zetu,” amesema Prof. Ngaruko aambaye ni gwiji katika uchumi na maendeleo nchini.

Naye Makamu Mkuu wa chuo ambaye pia ni mjumbe wa jukwa hilo, Prof. Elifas Bisanda, amewataka wajumbe wengine wa jukwaa hilo la Maprofesa kuwa viongozi kitaaluma ili kuwa mfano bora kwa wasomi wengine wote ambao wanaowaangalia wao kama kioo na dira ya mafanikio.

“Tunapaswa tuwe kioo halisi cha jamii yetu, tuhakikishe tunaongoza wengine katika kufanya tafiti na kutoa mihadhara yenye tija, tuwaongoze wanaotutazama katika kutafuta miradi na kusimamia vyema kazi za kitaaluma,” amesema Prof. Bisanda.

Prof. Modestus Varisanga, na mjumbe wa jukwaa hilo amesema, pamoja na majukumu mengine ya jukwaa la Maprofesa wa OUT mojawapo ni kuwakutanisha maprofesa wa chuo hiki na kukumbushana wajibu wao kwa jamii kutokana na ukweli kwamba, wasomi wanapaswa kufanya tafiti na kuja na majibu ya changamoto zinazoikabili jamii. Hivyo, amesisitiza kwa wajumbe wa jukwaa hilo kufanya tafiti na kuandaa mihadhara yenye kuibua na kutoa majawabu ya changamoto zilizopo kwenye jamii ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mada mbalimbali zimewasilishwa na maprofesa wa OUT akiwemo nguli wa sheria Prof. Alex Makulilo ambaye ni guru katika sheria za TEHAMA na mitandao, akiwemo na Prof. George Oreku ambaye ni gwiji katika ICT na "Cyber Security" nchini. Sambamba nao walikuwepo maprofesa washiriki wapatao tisa ambao kila mmoja ametoa mchango wa namna jukwaa la Maprofesa wa OUT linavyoweza kuwa kiongozi katika kutatua changamoto za jamii kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kuiunga mkono serikali katika jitihada kubwa inayofanywa kuwaletea wananchi maendeleo.

Post a Comment

0 Comments