Ticker

6/recent/ticker-posts

WAJASIRIAMALI WAFURAHISHWA NA HUDUMA ZA TBS KWENYE MAONESHO YA OSHA JIJINI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WAZALISHAJI wakiwemo wajasiriamali na wananchi kwa ujumla wamefurahishwa na elimu ambayo imetolewa na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika Maonesho ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wameahidi kutumia elimu hiyo kuleta matokea chanya ndani ya jamii.

Hayo yalisemwa na baadhi ya wazalishaji, wajasiriamali na wananchi waliotembelea Banda la TBS kwenye maonesho ya OSHA yaliyoanza Aprili 23 hadi 30, jijini Arusha.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wajasiriamali walisema wamepatiwa elimu kuhusu taratibu za kufuata ili kudhibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha ili ziweze kupata nembo ya ubora ya TBS.

Asha Abdallah, alisema amepata mwamko zaidi wa kuthibitisha ubora wa bidhaa anazozalisha, kwani ameambiwa kuwa huduma hiyo inatolewa bure kwa wajasiriamali kwa gharama za Serikali.

Aidha, baadhi ya wananchi walisema kupitia elimu waliyoipata itawaongezea umakini wa kuangalia muda wa mwisho wa matumizi kwa bidhaa wanayotaka kununua, kwani sasa wanaelewa kwamba bidhaa zilizoisha muda wa matumizi ni hatari kwa afya.

"Uwepo wa TBS kwenye maonesho haya imekuwa ni fursa muhimu kwetu, watu wengi wananunua bidhaa bila kuangalia muda wa mwisho wa matumizi ulioandikwa kwenye vifungashio, lakini kuanzia sasa nitakuwa balozi mzuri," alisema Paul Edward.

Akizungumza leo Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Mariam Maarufu alisema kupitia maonesho hayo imekuwa fursa muhimu kwa shirika kukutana na wadau mbalimbali na kuwaelezea majukumu yanayotekelezwa na TBS.

Mbali na kuwaeleza majukumu hayo, lakini pia wametoa elimu kwa wajasiriamali hao jinsi ya kuzalisha bidhaa bora ili waweze kupata alama ya ubora, ambayo itawafungulia wigo wa masoko la ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Maarufu,alama ya ubora ya TBS itawasaidia wajasiriamali na wazalishaji kwa ujumla kuaminika sokoni na kukubalika, hivyo kuingia kwenye soko kifua mbele, kwnai bidhaa zao haziwezi kutiliwa shaka.

Aidha, aliwataka waingizaji wa vipodozi nchini, kuingiza vipodozi ambavyo vimesajiliwa na TBS ambapo kwa kutembelea tovuti ya shirika hilo, wataweza kupata orodha ya vipodozi ambavyo haviruhusiwi kuingia nchini na vile vinavyoruhusiwa.

Alisema hatua hiyo itawezesha kuwaepusha kupata hasara, kwani wanapoingiza vipodozi vilivyopigwa marufuku watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria, ikiwemo bidhaa hizo kuzirudisha walikozitoa au kuteketezwa kwa gharama zao.

Alisema TBS ili kuhakikisha inalinda usalama wa wananchi imetoa namba yake kupiga bure ili kuripoti bidhaa ambazo ziko sokoni zenye kutiliwa shaka ambayo ni 0800 110 827.

Post a Comment

0 Comments