Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAHIMIZWA KUHAMA MAENEO HATARISHI

NA. MWANDISHI WETU

Wananchi wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari na kuondoka katika maeneo hatarishi yenye viashiria vya kuathiriwa na maafa ili kuendelea kuwa na jamii salama na tulivu hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Hayo yameelezwa hii na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na maafa ya mafuriko yaliyotokea tarehe 25 Aprili, 2024 katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo Kata ya Saranga, Mji Mpya na Kimochi ziliathiriwa na maafa hayo.

Dkt. Yonazi ametoa rai kwa wananchi kuzingatia taarifa zinazotolewa na Serikali pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari za mapema ili kuendelea kujilinda na kuendelea kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya maafa.

“Serikali itaendelea kukabiliana na maafa mbalimbali nchini kwa kuendelea kutoa elimu juu ya namna ya kujiandaa na kukabili maafa ili kuondokana na madhara yatokanayo na maafa pindi yanapotokea,” alisema Dkt. Yonazi.

Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya masuala ya menejimenti ya maafa hivyo itaendelea kuratibu kwa weledi na kuyafikia malengo kama inavyotakiwa.

Aidha alihimiza uongozi wa Mkoa kuendeleza juhudi katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya maafa pamoja na kuendelea kuwatumia wataalamu wa masuala ya Ustawi wa jamii lengo ni kutoa huduma za kisaikolojia kwa waathirika wa maafa hayo ili kuondokana na madhara waliyoyapata na kuweza kurejea katika hali zao na kujiletea maendeleo yao ya kila siku.

“Tutaeendelea kushirikiana na mkoa wa Kilimanjaro ili kuona hatua bora za urejeshaji wa hali na kipekee niendeleee kuupongeza uongozi wa Mkoa huu kwa hatua mlizochukua toka maafa yalipotokea niwasihi kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya majanga na maafa,”alisisitiza

Akitoa taarifa ya hali ya maafa kwa Katibu Mkuu huyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bi.Mwajuma Nasombe amesema kuwa, maafa hayo ya mafuriko yaliathiri Kata mbili ikiwemo ya Saranga na Mji Mpya zilizopo Manispaa ya Moshi na kusababisha athari kwa Kaya 283 zenye jumla ya watu 1195.

“Jumla ya nyumba 51 na kifo cha mkazi mmoja kilitokea katika maeneo ya Mji Mpya ambapo nyumba 35 zilibomoka kuta, nyumba 15 kuvyunjwa na maji pamoja na nyumba moja kubomoka kabisa”alieleza

Aidha alisema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya tathimi ya kujua maeneo yaliyoathirika, kutoa huduma na misaada ya kibinadamu, kutenga maeneo ya maalum ya kuwahifadhi (kambi maalumu) ili kuwapatia mahitaji waathiriki wa maafa hayo.

“Kati ya Kaya 283 ni Kaya 28 zilihifadhiwa katika makambi ila hadi leo ni kaya 12 tu zimebakia hapa kambini ambapo zingine zimepatiwa mahitaji yao muhimu na kuondoka kwenye makambi hivyo Serikali itaendelea kuwahudumia ili kuhakikisha hatua hii muhimu ya kurejesha hali inaendelea,” alieleza Mkurugenzi Mwajuma

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa Kati hizo zilizoathiriwa na mafuriko hayo huduma za msingi zimeendelea kutolewa ikiwemo misaada ya kibinadamu lengo kuwasaidia kuendelea kuwa na unafuu kutokana na madhara ya maafa hayo.

“Maafa haya yameleta madhara kwa baadhi ya miundombinu ikiwemo ya umeme na maji, uhalibifu wa baadhi ya vifaa katika Zahanati, baadhi ya mashamba yamesombwa na maji pamoja na vifo vya mifugo hivyo Serikali itaendelea kuwafikiwa wananchi ili kuhakikisha wanapata misaada zaidi ikiwemo kuendelea kuwahudumia na kurejesha hali,” alieleza Nzunda

Aidha Mkoa umeendelea na hatua mbalimbali ikiwemo kutoa rai kwa wananchi walio katika maeneo hatarishi kuhama, kuweka alama maalumu katika maeneo yote hatarishi pamoja na kuelimisha umma katika kukabiliana na madhara ya maafa mbalimbali.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (mwenye shati la batiki) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro Mhe. Zephania Sumaye (mwenye kaunda suti ya blue) wakiangalia athari za mafuriko katika Mto Rau uliopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua na kujionea hali ya madhara ya maafa ya mafuriko katika mkoa wa Kilimanjaro, ametembelea tarehe 2 Mei, 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu akizungumza wakati wa kikao cha utangulizi kabla ya ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi mkoani humo iliyolenga kukagua na kujionea hali ya madhara ya maafa ya mafuriko katika mkoa wa Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (mwenye shati la batiki) pamoja na timu aliyoongozana nayo wakiangalia athari za maafa baada ya tope na mawe kutoka katika mlima kuporomoka na kusababisha vifo vya watu wanne katika Kata ya Kimochi Kijiji cha Lyakombila Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kujionea madhara hayo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi  (kushoto) akimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Tixon Nzunda alipotembelea ofisini kwake kabla ya ziara yake ya kukagua na kujionea hali ya madhara ya maafa ya mafuriko katika mkoa wa Kilimanjaro.
wa Wilaya ya Kilimanjaro Mhe. Zephania Sumaye akizungumza na baadhi ya waathirika wa mafuriko mkoani humo waliohifadhiwa katika kambi ya shule ya msingi Ghona wakati wa  ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi iliyolenga kukagua na kujionea hali ya madhara ya maafa ya mafuriko katika mkoa wa Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi  (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro Mhe. Zephania Sumaye  (mwenye kaunda suti ya blue) pamoja na timu aliyoongozana nayo wakiwa katika ziara kukagua madhara ya maafa yaliyosababishwa na mvua katika maeneo ya Kata ya Kimochi Kijiji cha Lyakombila Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kujionea madhara hayo.

Muonekano wa baadhi ya nyumba zilizoathiriwa na maafa ya maporomoko ya tope na mawe kutoka milimani iliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Kata ya Kimochi Kijiji cha Lyakombila Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kujionea madhara hayo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi pamoja na timu aliyoongozana nayo wakizungumza na baadhi ya waathirika wa maafa ya mafuriko walio katika kambi ya muda ya Lucy Lameck walipohifadhiwa kwa ajili ya kupata huduma na mahitaji ya kibinadamu mkoani Kilimanjaro.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)




Post a Comment

0 Comments